Klabu ya Simba ipo mbioni kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Zanzibar Heroes, Kassim Khamis Ahmada ambaye ameonyesha kiwango bora katika michuano ya Kombe la Chalenji ambayo inaendelea nchini Kenya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe amenukuliwa akisema kuwa kila kitu kinakwenda vizuri na wanatarajia kumalizana na mchezaji huyo muda wowote kuanzia leo Alhamisi.

Dirisha dogo la usajili nchini Tanzania linatarajiwa kufungwa Ijumaa Desemba 15, mwaka huu, hivyo kama Simba wanahitaji kuwa na mchezaji huyo ni lazima wakamilishe dili hilo kabla ya siku hiyo kupita.

Akiufafanua kuhusu suala hilo, Hans Poppe amenukuliwa akisema: “Tunataka kufukuzana na muda kwa sababu dirisha linafungwa Ijumaa, kwa hiyo tutahakikisha baada ya mechi ya nusu fainali dhidi ya Uganda anasaini fomu za kuichezea Simba kuanzia ligi itakapoendelea na huo kuwa usajili wetu wa tatu baada ya Jonas Sakuwah na Asante Kwasi.”

Straika huyo anayeitumikia Klabu ya Tanzania Prisons ya jijini Mbeya, amecheza mechi mbili pekee kwenye mashindano hayo kabla ya kuumia na kukosa mechi mbili zingine. Katika mechi hizo alizocheza, amefunga mabao mawili dhidi ya Rwanda na Kilimanjaro Stars.

Kocha Msaidizi wa Simba, Mrundi, Masud Djuma, amesema katika kufuatilia kwake michuano hiyo, katika wachezaji wazawa amevutiwa na Khamisi kutokana na uchezaji wake pamoja na ushirikiano na wenzake anapokuwa uwanjani.

Haji Mwinyi Ngwali kuikosa The Cranes Kesho
Tanzania yatofautiana na Trump