Mahakama nchini Ujerumani imemhukumu kifungo cha maisha, muuguzi wa hospitali aliyekutwa na hatia ya kuwauwa kwa makusudi wagonjwa 85 waliokuwa chini ya uangalizi wake, kwa kuwasababishia mshituko wa Moyo.
Mahakama ya mji wa Oldenburg iliyopo Kaskazini mwa Ujerumani imemkuta na hatia muuguzi huyo, Niels Hoegel mwenye umri wa miaka 42, ya kuwauwa wagonjwa wake kwa kuwachoma Sindano ya sumu kati ya mwaka 2000 na 2005 alipofumwa akifanya uhalifu huo.
Polisi wamesema kuwa huenda, Hoegel aliangamiza maisha ya wagonjwa zaidi ya 200. huku Waendesha mashitaka walilazimika kuifukua miili ya watu 130 katika kukusanya ushahidi.
Mahakama haikuweza kuthibitisha idadi kamili ya wahanga wa mtu huyo, kwasababu miili ya marehemu wengi ilichomwa moto kabla ya kufanyiwa uchunguzi.
Jaji wa mahakama ya Oldenburg, Sebastian Buehrmann amesema ni vigumu kuelewa sababu ya mlolongo huo wa mauaji, ambayo amesema yamepitiliza kile ambacho binadamu anaweza kukielewa.
Pia, Buehrmann vile vile ameomba radhi kwa familia za wahanga, kwasababu mahakama haikuweza kupata majibu kwa masuala yote yanayoulizwa kuhusu uovu huo.
Hata hivyo, siku ya mwisho ya kusikilizwa kesi dhidi yake, muuaji huyo, Niels Hoegel ameomba msamaha kwa matendo yake aliyokiri kuwa ni ya kutisha.