Mgombea Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Upinzani Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (LAMUKA), Martin Fayulu ameyakataa matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.
Fayulu ambaye ni miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini humo, ameyagomea matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) ambayo yanaonyesha kuwa Felix Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na kutangazwa mshindi mteule wa urais.
Tshisekedi alipata zaidi ya kura milioni 7, naye Fayulu akapata kura takriban milioni 6.4 huku mgombea wa serikali Emmanuel Ramazani Shadary akimaliza wa tatu akiwa na takriban kura milioni 4.4.
“Hii ni kashfa mbaya sana, matokeo haya hayana uhusiano hata kidogo na ukweli halisi, raia wa Congo hawataukubali utapeli kama huu daima, Felix Tshisekedi hakupata kura milioni 7, haiwezekani, amezitoa wapi?”amehoji Fayulu alipokuwa akifanya mahojiano na BBC
Aidha, hapo awali, Martin Fayulu alisema kuwa matokeo hayo ni mapinduzi halisi kupitia uchaguzi na akatoa wito kwa waangalizi wa uchaguzi kuchapisha matokeo waliyo nayo aliyosema ni ya kweli.
kwa upande wake, Felix Tshisekedi akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika mji mkuu Kinshasa amesema kuwa atakuwa rais wa raia wote wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
-
Mpinzani atangazwa mshindi uchaguzi wa Urais DRC
-
Ulinzi mkali wazua jambo matokeo ya urais DRC
- Mpinzani atamba kushinda Urais DRC, Marekani yatuma jeshi
Hata hivyo, kumekuwa na tetesi kwamba ucheleweshwaji wa shughuli ya kutangaza matokeo, ambayo awali yalitarajiwa kutangazwa Jumapili, kulitoa muda kwa Rais Kabila na Tshisekedi kukutana na kufanya mazungumzo maalum ya makubaliano.