Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema kukamilika kwa ujenzi wa meli ya MV Mwanza na Ukarabati wa meli ya MV Umoja kutarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa mikoa inayozunguka Mkoa wa Mwanza pamoja na nchi Jirani zinazotumia Ziwa Victoria.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwakibete ameyasema hayo jijini Mwanza mara baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati na ujenzi wa meli hizo kusema Serikali itaendelea kutenga fedha ili kukamilisha miradi yote ya Kampuni ya Huduma za Meli.

“Nipende kuwahakikishia kuwa kukamilika kwa ujenzi wa meli ya MV Mwanza  kutatochea sana uchumi na kuongeza pato kwa mikoa inayozunguka Ziwa lakini pia kukamilika kwa ukarabati wa MV Umoja kutarahisisha sana usafiri wa abiria na mizigo”, Amefafanua Naibu Waziri Mwakibete.

Aidha Naibu Waziri Mwakibete ameitaka Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuhakikisha inawasimamia kwa karibu Wakandarasi wote wawili wanaotekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati ili wakamilishe miradi hiyo kwa kuzingatia thamani ya fedha lakini kuongeza ujuzi kwa wataalaam wa ndani.

Naibu Waziri Mwakibete ameihakikishia MSCL kuwa changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo upungufu wa watumishi wa fani za uhandisi kuwa litashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi ili kufanya taasisi hiyo iweze kuwa imara kiutendaji.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa MSCL, Philemoni Bagambilana, amemuhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa taasisi imejipanga na inasimamia kwa karibu miradi hiyo ili kuleta matokeo ya uwekezaji unaofanywa na Serikali katika ukanda huo.

Bagambilana ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye taasisi hiyo na kusema moja ya matokeo ya uwekezaji kwenye ukarabati wa meli hasa za MV Victoria na MV Butiama ni kuongezeka kwa mapato kutoka bilioni takribani 1 kwa mwaka 2019 hadi kufikia bilioni takribani 4.5 mwaka 2021.

Mradi wa Ujenzi wa Meli ya MV Mwanza unatekelezwa na Kampuni ya Gas Entec Company Limited na Kampuni ya KANGNAM Corporation kwa kushirikiana na SUMA JKT kwa gharama ya shilingi bilioni 96.9 na ukarabati wa Meli ya MV Umoja unatekelezwa na SM Solution Co ltd ya nchini Korea na unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 19.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 18, 2022
Miss World 2021 apatikana