Magwiji wa soka Barani Afrika klabu ya Al-Ahly SC imemsimamisha mfungaji bora wa kikosi chao, Mahmoud Kahraba kwa mwezi mmoja pamoja na faini nzito ya EGP 200,000 sawa na Shilingi milioni 30 za Tanzania baada ya kuripotiwa kubishana na Kocha wake Pitso Mosimane.
Kosa lingine lililomuingiza hatiani mshambuliaji huyo ni kudaiwa kuhudhuria harusi bila kumjulisha msimamizi wa timu huku akishindwa kuzingatia taratibu za Ugonjwa na Corona (COVID19) na akafika kwa kuchelewa katika mazoezi ya timu.
Kahraba kwa sasa ndiye mfungaji bora wa Ahly msimu huu akiwa na mabao sita na Assist moja katika michezo 14 kwenye Michuano yote, lakini mshambuliaji huyo amekutwa na utovu wa nidhamu mara kadhaa.
Miezi michache iliyopita alitozwa faini EGP milioni moja sambamba na kufungiwa michezo kumi na mbili msimu adhabu iliyotolewana chama cha soka nchini Misri ‘EFA’.
Kama hiyo haitoshi mamlaka za soka nchini Sudan zimemtuhumu Kahraba kwa ubaguzi wa rangi dhidi ya mchezaji wa Al Merrikh wakati wa mchezo wa hiyo timu zote mwezi uliopita, jambo ambalo baadae lilikanushwa na klabu hiyo ya Sudan.
Taarifa fupi kutoka ndani ya klabu haijaonyesha nini Kahraba amefanya, lakini ripoti ziliibuka zikisema kwamba winga huyo alikuwa na ugomvi na kocha mkuu Pitso Mosimane, alikataa kupeana mikono na kuzungumza na Kocha huyo Kutoka Afrika Kusini kwa namna ya utovu wa nidhamu.
Kulingana na ripoti, tabia hii ilimkasirisha Pitso Mosimane, ambaye alikuwa na mkutano na mkurugenzi wa Klabu, Sayed Abdel-Hafiz na akaomba adhabu nzito kwa mchezaji huyo, licha ya Kahraba kuomba msamaha kwa kocha mkuu.
Kahraba sasa atakosa michezo minne ijayo za Al Ahly dhidi ya AS Vita Club (michezo miwili), Al-Merrikh, na Ismaily.
Kahraba alisajiliwa na Al Ahly Januari 2020 akitokea kwenye klabu ya Aves ya Ureno, na tangu wakati huo amefunga mabao 12 katika michezo 38 kwenye mashindano yote.