Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa UDA-RT, Deus Bugaywa amesema mabasi 29 kati ya mabasi 140 ya mradi huo yameharibika kutokana mvua kubwa zilizonyesha mfululizo jijini Dar es salaam.
Bugaywa amesema kutokana na kujaa maji katika ofisi za mradi huo zilizopo Jangwani baadhi ya wafanyakazi wamepewa likizo mpaka maegesho ya mabasi hayo yatakapopatikana.
Ameongezea kuwa moja ya sababu iliyochangia hali hiyo ni sehemu ya ukuta ya eneo hilo kudondoka na hivyo maji ya mto Msimbazi kuingia ndani kwa wingi.
Aidha amesema kuwa matengenezo ya mabasi hayo yanafanyika eneo la maegesho ya muda katika vituo vya Gerezani, Kivukoni na Kimara wakati wakiendelea kutafuta sehemu nyingine.