Mvutano wa hoja umeibuka bungeni leo baada ya Zainabu Katimba, Mbunge wa Viti Maalimu (CCM), kushauri yafanyike Marekebisho ya Sheria ili kuongeza adhabu ikiwemo kuhasiwa, kwa wale watakaothibitika kwamba wamefanya Kosa la Ubakaji.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Adelardus Kilangi, amesema kuwa adhabu iliyopo juu ya wabakaji inatosha, kwani katiba ya nchi hairuhusu mtu kuteswa ama kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.

“Pendekezo la kuhasiwa kwa mbakaji tutavunja katiba kwa sababu, katiba inaeleza ni marufuku mtu kuteswa kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza/kumdhalilisha, nafikiri adhabu zilizopo zinajitosheleza kwa sasa” amesema Dkt Kilangi.

Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria amempongeza Mbunge Zainabu kwa kusimamia haki za watoto na wanawake na kusema, katika kutoa ushaidi, wameondoa vigezo vilivyokuwepo ikiwa ni pamoja na kutoruhusu mtoto aliyefanyiwa ukatili kutoa ushaidi Mahakamani.

Amesema, adhabu zilizopo mpaka sasa ni kali ikiwemo miaka 30 na kwamba, kama itabidi kuongeza adhabu kama ambavyo Mbunge alivyoshauri, basi bunge likae pamoja.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, akiongezea katika jibu la Mwanasheria Mkuu, ameendelea kuwasisitiza wazazi na walezi, kujenga ukaribu na watoto wao ili kuweza kuwaambia pale wanapokutana na vitendo vya ukatili.

“Hata tuwe na sheria kali kiasi gani hatutamaliza tatizo la ubakaji na ulawiti kwa watoto na wanawake, nitoe msisitizo kwa wazazi na jamii kutimiza wajibu wetu wa malezi na ulinzi kwa watoto, mtoto anabakwa miezi mitatu bila mzazi kujua unajiuliza je huyu ana wazazi?” amesema Waziri Ummy.

Bukina Faso: Bunge lapitisha wananchi kupewa silaha waingie vitani
Jina la mkongwe Giorgio Chiellini latua UEFA

Comments

comments