Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Tanzania Prisons Jackson Mwafulango amesema timu yao imekua ikipewa hukumu nzito ya kucheza kwa kukamia michezo ya Ligi Kuu, jambo ambalo sio halali kwao.
Mwafulango amesema Tanzania Prisons imekua inahukumiwa hivyo kwa sababu ambazo hazina mashiko, lakini kiufundi kikosi chao kimekua kikicheza soka safi.
Amesema kikosi chao kinapokua kwenye michezo inayowakutanisha dhidi ya klabu za Simba SC na Young Africans kimekua kikipata wakati mgumu wa kukamiwa kwa na kuchezewa rafu za makusudi.
“Wakiwa wanajiandaa kucheza na Tanzania Prisons mazoezi yao huwa yanabadilika, wachezaji wao watapigwa miguuni na mambo mengine, watawaumiza bure jamani, sisi tunacheza mpira, kwa hiyo unakuta mwisho wa siku Game inakua tafu,”
“Wakija kuona mambo yanakua tofauti viongozi, wachezaji na mashabiki wao wanasema ndio yale yale, kumbe wao wenyewe wanafanya mazoezi mengi magumu kuja kucheza na sisi.”
“Tunacheza na Simba SC tarehe 26 Mbeya, nenda kwenye mazoezi yao kuelekea huo mchezo ukaangalie, utakua watu wanaambiwa Fika Fika Fika wale wanafika sana, unakuta mtu anahangika, wanakuja wametukamia.”
“Sisi ni jeshi, timu yetu inafanya mazoezi ya Fiziki, muda wote unakuta tupo FIT, hata ule mchezo na Yanga wakisema turudie sasa hivi hapa hawapati goli, kwa sababu tupo vizuri.” amesema Mwafulango.