Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema katika mwaka mmoja wa madaraka ya Rais Samia Suluhu Hassan, sekta ya afya imefanikiwa kuhudumia wagonjwa wengi wa magonjwa tofauti na kupunguza vifo kutikana na kuboreshwa kwa huduma za afya.
Ameyasema hayo leo March 4, 2022, katika taarifa yake ya mafanikio ya Wizara ya Afya kuelekea mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani.
Waziri Ummy amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutoa kipaumbele kikubwa katika Sekta ya Afya katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuingia madarakani ambapo jumla ya shilingi Bilioni 891.5 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Wizara ya Afya.
“Miradi ya maendeleo ya kipaumbele iliyotekelezwa moja kwa moja na Wizara ya Afya ni pamoja na Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali Maalumu na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo kiasi cha shilingi bilioni 90.4 zilitolewa,” amesema Waziri Ummy.
Ametaja pia Ukarabati wa majengo ya kufundishia katika Vituo vya Afya ambapo kiasi cha shilingi Bil. 6.3 kimetolewa. Ununuzi na usambazaji wa Dawa, Vifaa, Vifaa tiba na vitendanishi, ambapo jumla ya shilingi Bil. 333 zimetolewa.
Fanikio la kununua Vifaa Tiba vya Uchunguzi, kuimarisha huduma za upatikanaji wa damu salama pia ni mfano alioutaja.
Pia amesema serikali imeweza kugharamia posho za wanafunzi watarajali (Intens) wa Udaktari, Udaktari wa Meno na wataalam wa Afya Shirikishi kiasi cha shilingi Bil. 49.9 zimetolewa.
“Kulipia gharama za masomo kwa ajili ya Madaktari bingwa (specialists) na Madaktari bingwa Bobezi (Super Specialists) ndani na nje ya nchi ambapo jumla ya shilingi Bil. 4.4 zimetolewa,” ameongeza waziri Ummy.
Wizara pia imeweza kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (ikiwemo ununuzi wa dawa ARVs, Dawa za Malaria na Vitendanishi) ambapo kiasi cha shilingi bilioni 117 kimetolewa.
“Kuboreshwa kwa Miundombinu ya kutolea Huduma za Afya na Kuimarika kwa Upatikanaji wa Huduma za Matibabu ya Ubingwa Bobezi (Super specialized) nchini,” ameongeza Waziri Ummy.
Pia ameongeza, Kuimarika upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa Tiba, vitendanishi katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya.
Kuimarika kwa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto na Kundelea kupunguza Idadi ya Wagonjwa na Vifo vinavyotokana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu.