Uongozi wa Young Africans umepasua ukweli wa usajili wa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia na klabu ya Zanaco FC Moses Phiri, ambaye anadaiwa atakuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo kuanzia mwezi huu Januari.
Moses Phiri anatajwa kuwa sehemu ya wachezaji waliosajiliwa klabuni hapo katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili, ili kuongeza chachu ya kufikia malengo ya kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara na Kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao 022/23.
Makamu Mwenyekiti wa Young Africans Frederick Mwakalebela amesema suala la Phiri kujiunga na kikosi chao ni suala la muda kwa kuwa linashughulikiwa kwa weledi mkubwa.
“Usajili wa Phiri, upo katika mchakato mzuri kwa sababu tumefikia katika wakati mzuri ambao naamini utakamilika kwa kuwa upo chini ya watu makini ambao wanasimamia suala hilo.”
“Sisi hatutaki kuwa waongeaji, nadhani mashabiki wenyewe wamekuwa wakijua namna tunavyofanya mambo yetu ingawa kwa sasa bado tunapambana kupata winga mwingine kutokana na wingi wa mejeruhi waliopo kwenye kikosi chetu,” amesema Mwakalebela.
Phiri anatamba rekodi ya kufunga mabao 17 katika Ligi Kuu ya Zambia msimu uliopita, huku akiwa sehemu ya kikosi cha Zanaco FC kilichotinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2021/22.