Bondia Hassan Mwakinyo amesema amejiandaa vyema kupambana na Peter Bobson wa Marekani katika Pambano la kuwania Mkanda wa WBC, litakalopigwa Desemba 30 mjini Unguja, Visiwani Zanzibar katika viwanja wa Mao tse Tung.
Mwakinyo atapanda ulingoni visiwani humo kwa mara ya kwanza, baada ya Serikali ya Zanzibar ‘SMZ’ kuruhusu mchezo wa Masumbwi kurindima katika visiwa hivyo, baada ya kimya cha muda mrefu.
Akizungumza kuhusu maandalizi yake kuelekea Pambano hilo, Bondia huyo kutoka Tanga amesema, anataka kulitumia pambano hilo kuandika historia ya kuwa bondia wa kwanza kupigana tangu kuruhusiwa mchezo wa masumbwi visiwani Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mwakinyo amesema katika Pambano hilo ambalo lipo chini uratibu wa promota Shomari Kimbau, atahitaji kurejesha heshima yake na ya Tanzania katika uso wa Dunia.
Kwa upande wa Mratibu Shomari Kimbau amesema Bobson kutoka Marekani yupo katika hadhi ambayo inalingana na ya Mwakinyo na kwamba anatarajia Pambano hilo litakuwa na ushindani mkali.
Amesema ameamua kuliandaa pambano hilo visiwani Zanzibar ili kuandika historia ya kurejeshwa masumbwi tangu yalipopigwa marufuku.