Bondia Hassan Mwakinyo amemvaa bondia mstaafu, Rashid Matumla akieleza kuchukizwa na hatua ya mkongwe huyo kumkosoa vikali kocha wake kuhusu pambano la hivi karibuni dhidi ya Mfilipino, Arnel Tinampay.
Kupitia kipande cha sauti ambacho Mwakinyo amejitambulisha kabla ya kufunguka ya moyoni, amesema angetegemea kuona mzee Matumla kama Mtanzania akifurahia ushindi badala ya kumvaa kocha wake.
Ameeleza kuwa Matumla hakuwa kocha bora kwa watoto wake na kwamba hiyo ndiyo sababu watoto wake hawakufanya vizuri kwenye tasnia ya masumbwi.
“Binafsi mimi nilikuwa nakuheshimu sana Matumla, lakini kwa kitendo ulichokifanya umepoteza heshima kwangu. Na nimefanya hivyo kwa maana sihitaji tena kuja kufanya pambano na Azam halafu wakamuweka kama mchambuzi,” anasikika Mwakinyo.
Mzee Matumla alikuwa mmoja kati ya wachambuzi wa pambano hilo lililoshuhudiwa Desemba 29, 2019 katika Uwanja wa Uhuru na kurushwa moja kwa moja na kituo cha runinga cha Azam.
“Matumla alikuwa anaongea kimajungu kiasi kwamba uongeaji wake amefanya watu wengi walioangalia lile pambano kwenye TV waamini kwamba nimepoteza kwa kuwa alikuwa ananikosoa kama kwamba sijui kupigana. Nimechukia sana, na Watanga wamechukizwa. Na ninaomba nikuthibitishie tu kwa wingi wa watu niliokuwa nao hatumtaki tena Matumla kama mchambuzi,” ameeleza.
Mchambuzi huyo alikosoa mara kadhaa kitendo cha Mwakinyo kuendelea kukaa kwenye kamba na kumpa nafasi mpinzani wake kurusha makombora kadhaa, akidai kuwa kocha wake alipaswa kumueleza hilo. Lakini pia kitendo cha watu wengi kuonekana kwenye kona ya Mwakinyo alikieleza kuwa ni moja ya vitu ambavyo vinamchanganya kwani anapokea maelekezo mengi kwa wakati mmoja. Aligusia pia makosa aliyoyaona ya kiufundi na kikufunzi.
Kutokana na ushindi dhidi ya Tinampay, Mwakinyo amepewa nyota nne, ni bondia anayeshikilia nafasi ya 19 duniani kwenye uzito wa Super Welterweight, na nafasi ya kwanza kwa Afrika.