Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo ameporomoka kwenye viwango vya ubora duniani kutoka nafasi ya 90 mpaka 105.
Mwakinyo mwenye nyota mbili na anayepigana kwenye uzito wa Super Welter duniani anashika nafasi ya 105 kutoka 90 kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Box Rec yenye maskarni yake Uingereza.
Taarifa hiyo inakuja ikiwa ni wiki kadhaa toka bondia huyo kugoma kupanda ulingoni kupigana na Jullius Indongo akidai kukiukwa kwa mkataba wake na Promota wake Karigo Godson.
Kitendo hicho kilifanya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kumfungia mwaka mmoja na faini ya shilingi milioni moja.
Kwa mujibu wa Box Rec, mabondia wengine wa Tanzania, Twaha Lubaha Kiduku’ na Abdallah Pazi Dulla Mbabe pia wameshuka kwenye viwango vya ubora katika uzito wa Super Middle.
Kiduku aliyekuwa akishika nafasi ya tano ameporomoka mpaka nafasi ya 13 huku Dulla Mbabe akishuka mpaka nafasi ya 36 kutoka 14.
Bondia mkongwe hapa nchini, Rashid Matumla amesema kupanda na kushuka kwenye viwango vya ubora kwa mabondia ni jambo la kawaida wanachopaswa kufanya ni kupambana na kurejea kwenye ubora wao.