Bondia Bora Barani Afrika Hassan Mwakinyo, amewataka wadau wa mchezo wa Masumbwi Tanzania kuupa heshima mchezo huo.
Mwakinyo ambaye anashika nafasi ya kwanza Barani Afrika kwa sasa, ametoa rai hiyo alipohojiwa na Clouds FM kupitia kipindi cha Sports Extra jana Jumanne (Agosti 31).
Mwakinyo amesema wadau wa masumbwi Tanzania wanauchukulia kirahisi mchezo huo kwa kuweka ubishi usio na maana, kwa lengo la kujiridhisha nafsi zao.
Amesema umefika wakati kila mdau anapaswa kufahamu masumbwi ni mchezo wa ajira kama ilivyo michezo mingine duniani, na Bondia anapaswa kupambana kwa malengo ya kujiingizia kipato.
“Duniani kote sijawahi kusikia mabondia wanashindania magari, huwa wanapewa mikanda yenye thamani na pesa ndefu ambazo zitawafanya wanunue magari wanayotaka au wakawekeze kwenye viwanda vya magari baada ya pambano.”
“Mapromota wa Tanzania waupe thamani mchezo huu wa boxing.” amesema Mwakinyo
Mwakinyo anatarajia kupanda ulingoni Keshokutwa Ijumaa (Septemba 03), kuzichapa na Bondia kutoka Namibia Julius Indongo.
Pambano hilo litafanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.