Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa Na Michezo Harison Mwakyembe jioni hii amekabidhi bendera ya taifa kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys), ikiwa ni ishara wa kuanza safari ya kuelekea nchini Gabon ambapo zitapigwa fainali za Afrika kwa vijana.

Mwakyembe amekabidhi bendera ya taifa kwa nahodha wa Serengeti Boys dakika chache kabla ya kuanza kwa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi Ghana, ambao unachezwa katika dimba la taifa jijini Dar es salaam.

Baada ya kukabidhi bendera ya taifa, Waziri Mwakyembe aliwahusia vijana wa Serengeti Boys kwenda kupambana katika fainali hizo ili wafanikishe lengo la kutwaa ubingwa wa Afrika, sambamba na kufuzu kwa fainali za kombe la dunia zitakazofanyika baadae mwaka huu nchini India.

“Katika mechi zote ambazo tumewajaribu ndani na nje ya nchi, mmeonyesha ni vijana ambao mnaweza kuifanya hii kazi, kwa hiyo tunawaombeni wekeni mbele uzalendo, piganieni nchi yenu, na sisi Tanzania tutembee vifua mbele” Amesema Mwakyembe

Serengeti Boys itakwenda Rabat, Morocco kuweka kambi takribani mwezi mmoja kuanzia Aprili 5, mwaka huu. Ikiwa huko angalau itacheza michezo ya kimataifa ya kirafiki isiyopungua miwili dhidi ya wenyeji Morocco na timu nyingine ya jirani ama Tunisia au Misri. Kambi hiyo ya Morocco itamalizika Mei mosi, mwaka huu ambapo timu itasafiri hadi Cameroon.

Ikiwa Cameroon, timu itacheza michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya wenyeji yaani Mei 3 na 6, mwaka huu kabla ya kusafiri Mei 7, mwaka huu kwenda Gabon ambako Serengeti Boys imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.

Tanzania yasaini msaada wa Bilioni 490 kutoka Umoja wa Ulaya
Watumiaji wa Simu hatarini kupata ugonjwa wa akili