Baada ya tukio la utekaji wa wasanii wa muziki wa bongo fleva hapa nchini kutokea siku chache zilizopita na baadaye kupatikana, limesababisha kutanda kwa hofu kubwa miongoni mwa wasanii wa muziki huo hali ambayo imepelekea Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kujitokeza hadharani kulaani kitendo hicho na kuahidi kuwashughulikia wale wote waliohusika.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Waziri huyo amesema kuwa amesikitishwa sana na kitendo hicho hivyo ameahidi kulishughulikia jambo hilo kwa haraka zaidi ili wahusika wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria.
“Hiki kilichotokea siyo hali ya kawaida kwa watanzania, hatuwezi kukubali kitu kama hiki kiendelee kutokea,nitalifuatilia kwa ukaribu sana, nitajitahidi nipate majibu kabla ya bajeti yangu Bungeni”. Dkt. Mwakyembe
Hata hivyo Dkt. Mwakyembe amewataka wasanii wote nchini kutoa taarifa Ofisini kwake pindi tu wanapoona kuna tatizo au mtu yeyote anawasumbua kuhusu suala zima la sanaa kwani yeye ndiye Waziri mwenye dhamana na si mwingine.
Kwa upande mwingine, Mwakyembe ameongeza kuwa ameagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa haraka zaidi katika tukio hilo baya la utekaji kwani siyo la kawaida kutokea hapa nchini.
Pia Waziri huyo mwenye dhamana na wasanii ametoa ujumbe kwa vyombo vyote vilivyopo chini ya Wizara yake kutofanya mahojiano yoyote yanayowahusu wasanii hao bila ya kuwepo taarifa kamili kutoka kwake.