Waziri wa Sheria na Katiba, Dkt. Harrison Mwakyembe ametetea uamuzi wa Serikali kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani dhidi ya maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu nchini kubatilisha vifungu vinavyohalalisha ndoa kwa watoto chini ya umri wa miaka 18.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ulitokana na kesi iliyofunguliwa na taasisi kutetea haki za watoto ya ‘Msichana Initiative’, ikipinga vifungu vilivyo katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu msichana chini ya miaka 18 kuolewa ikiwa kuna ridhaa ya wazazi wake.

Akizungumza leo na ITV, Dk. Mwakyembe amesema kuwa dhamira ya Serikali ni nzuri na lengo lake halikinzani na lile la wanaharakati waliofungua kesi hiyo, lakini wanachohitaji ni kuwashirikisha wananchi wote kuwa na maridhiano na makubaliano hayo.

“Kitu kizuri pia hakikimbizwikimbwi. Watanzania tuna makabila mengi sana. Inabidi kuwa na maridhiano ya wote ili Tanzania iwe kisiwa cha amani,” alisema Dk. Mwakyembe.

“Sisi hatupingi hoja za msingi zilizotolewa, na sisi nia yetu ni moja. Lakini tumeshasema tunaanza mchakato wa White Paper ili kila mtanzania ashiriki kuibadili,” aliongeza.

Aidha, Waziri huyo wa Sheria na Katiba alisema kuwa nia nyingine ya Serikali ni kupata busara za Mahakama ya Rufaa juu ya uamuzi huo kwani maamuzi ya mahakama ya rufani hutumika kama sheria.

Dk. Mwakyembe alieleza kuwa Serikali pia inapinga ndoa  za watoto na imeshaanza mchakato wa kutaka kuibadili, lakini wanapopishana na waliofungua kesi hiyo ni njia tu ya kufikia uamuzi huo.

“Ni kweli hivyo vifungu vinakinzana na haki ya mtoto, tunachopishana ni njia ya kufikia hiyo hatma. Sisi kama Serikali tunataka kuwashirikisha Watanzania wote kufikia azma, wakati wenzetu kama wanaharakati, kwasababu wamepewa pesa ya kufanya hivyo wanataka iwe haraka hivyo,” alisema.

Alisema Serikali iko mstari wa mbele kupinga ndoa za utotoni na ndio sababu hivi karibuni Bungeni ilipisha sheria ya elimu inayotoa kifungo cha miaka 30 kwa mtu atakayemuoa mwanafunzi wa shule ya msingi au shule ya sekondari.

Mkurugenzi wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi alieleza kushangazwa na hatua ya Serikali kutangaza nia ya kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya Mahakama Kuu iliyobatilisha vifungu vinavyoruhusu ndoa ya mtoto chini ya miaka 18.

TRA yatangaza kukusanya kodi za nyumba za kupanga
Lissu awazidi kete mawakili wa Serikali Mahakamani, apewa dhamana