Mwalimu wa shule ya msingi Saint Leo, amejeruhiwa kwa kupigwa risasi kichwani na mfanyabiashara mmoja wilayani Igunga Mkoani Tabora, baada ya kujisaidia karibu na gari lake.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Hamisi Selemani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo ameeleza kuwa lilitokea Januari 15 mwaka huu. Alisema Jeshi la Polisi linamshikilia mfanyabiashara huyo aliyetajwa kwa jina la Felix Peter Msele.

Akielezea jinsi ambavyo tukio hilo lilivyotokea, Kamanda Selemani alisema kuwa Mwalimu Teophano Mvula ambaye ni mkazi wa mtaa wa Nkokoto kata ya Igunga alijisaidia karibu na gari la mfanyabiashara huyo karibu na bar moja na kwamba mfanyabiashara huyo alimfuata na kuanza kujibishana nae.

Alisema kuwa wakati mabishano hayo yakiendelea, mfanyabiashara huyo alitoa bastola na kupiga risasi moja hewani na risasi ya pili aliielekeza kwenye kichwa cha mwalimu huyo na kumjeruhi. Alieleza kuwa baada ya kuanguka chini, wasamalia wema walimchukua na kumkimbiza hospitalini.

Naye mganga Mfawidhi wa hospitali ya Wilaya ya Igunga, Abdallah Ombeni alithibitisha kumpokea Mwalimu Mvula akiwa na majeraha kichwani. Alisema alitibiwa na kushonwa nyuzi tatu kabla hajaruhusiwa kwenda nyumbani.

Kamanda Selemani ameeleza kuwa Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa pamoja na bastola yake nyenye risasi kumi na atafikishwa mahakamani.

 

Agundua ana ujauzito siku nne tu kabla ya kujifungua, fahamu mkasa wake
AT amuandikia ujumbe mzito Ali Kiba, afichua mengi kati yao