Mwalimu wa Shule ya Msingi Mwamakoye Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumchapa mtoto wake na kusababisha kifo chake.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 21 mwaka huu, saa kumi jioni na kumtaja marehemu kuwa ni Sifael Emmanuel (8) mwanafunzi wa shule hiyo.
 
Aidha, Msangi amesema kuwa taarifa zilizopatikana zinasema kuwa, mtoto huyo alikuwa na tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani pindi anapoagizwa dukani na mama yake.
 
“Kutokana na tabia hiyo mama yake alikuwa akimpatia adhabu, lakini hakukoma na kwamba juzi mtoto huyo aliagizwa tena dukani na kuendelea na tabia yake ile ile ndipo alipoanza kumshushia kipigo hadi kusababishia kifo,” amesema Msangi.
 
Ameongeza kuwa Kutokana na tukio hilo, wananchi walioshuhudia walitoa taarifa kituo cha polisi na baadaye mwalimu huyo alikamatwa na kupelekwa kituoni.
 
Hata hivyo, Msangi aesema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwamba, utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Ujenzi wa Kingo za Bahari washika kasi Jijini Dar
Vurugu zaibuka katika mkutano wa CUF Dar