Watanzania wametakiwa kuenzi fikra na falsafa zinazoishi za Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo na kuendelea kuwa funzo kwa vizazi vya sasa na vijavyo ikiwemo kuenzi rasilimali za Taifa na Utawala bora kwani misingi iliyowekwa tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza inasimamiwa mpaka sasa.

Wito huo, umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Dennis Mwila wakati wa Kongamano la miaka 20 ya Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliyoandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe na kufanyika Jijini Mbeya.

Amesema, “Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni kiongozi aliyeweka msingi wa uhuru wetu na kuimarisha nchi yetu na leo tunatambulika ulimwenguni kote kutokana na mchango wake mkubwa wa kuikomboa Tanzania na Afrika kwa ujumla wake” amesisitiza Homera.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambae pia alikuwa ni mtoa Mada Mkuu katika Kongamano hilo, Mzee Joseph Butiku amesema Mwalimu Nyerere ameacha mafundisho mengi katika utawala bora na usimamizi wa rasilimali za nchi.

“Sote ni mashahidi Mwalimu Nyerere katika maisha yake amekuwa akisisitiza misingi ya uongozi wa kiadilifu, uwajibikaji na ushirikiano wa wananchi katika kufikia malengo ya maendeleo. Leo, tunahimizwa kuchukua mafundisho haya kama mwongozo katika shughuli zetu za kila siku” Amesisitiza Mzee Butiku.

Awali, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha alisema Chuo hicho kinajivunia kuchangia kwa kiasi  kikubwa katika kuzalisha wataalamu wenye maadili na maarifa katika eneo la utawala na utawala bora.

Katika kongamano hilo, jumla ya mada ndogo sita ziliwasilishwa na wanazuoni wa Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ikiwa ni Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu masuala ya Ardhi, Wanawake, Madini, viwanda na kuongozwa na kaulimbiu isemayo “Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu utawala bora na ulinzi wa rasilimali za taifa kwa maendeleo endelevu.”

Watoto Njiti wapewa upendo nyanja za Elimu, Afya
Tanzania yatoa wito kwa Mataifa tajiri Duniani