Beki Sergio Ramos, amesema anaondoka katika cha kikosi Paris Saint-Germain (PSG) baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu 2022/23.
Beki huyo amesisitiza atafuata nyayo za Lionel Messi ambaye tayari ameshasema hatakuwepo katika kikosi hicho msimu ujao kwani anataka kuondoka klabuni hapo.
Ramos tayari ameshacheza ndani ya PSG kwa misimu miwili baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea Real Madrid.
Beki huyo amesema mechi ya mwishoni mwa juma lililopita ya Ligi Kuu ya Ufaransa dhidi ya Clermont Foot, ndio ilikuwa mechi yake ya mwisho kuitumikia PSG.
Ramos mwenye umri wa miaka 37, amekuwa mmoja wa wachezaji waliotoa mchango mkubwa wa kuisaidia timu kupata mataji ya Ligi Kuu ya Ufaransa mfululizo ambapo msimu huu amefunga mabao matano katika mechi 57 alizocheza msimu huu katika michuano yote.
“Kuvaa jezi za PSG kwa misimu miwili mfululizo imekuwa kitu kikubwa chenye mafanikio kwangu, ni misimu miwili ambayo sitakuja kuisahau katika maisha yangu lakini mikakati yangu ni kuondoka na kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.
“Juzi Jumamosi ndiyo ilikuwa mechi yangu ya mwisho ndani ya PSG na ilitumika kuwaaga mashabiki ambao walikuwa wakinisapoti tangu nilipotua Ufaransa mara ya kwanza,” amesema.
Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi amesema anamshukuru Ramos kwa ushirikiano aliouonyesha kwa viongozi na wachezaji wote, hivyo anamtakia mema katika maisha yake mapya.