Baada ya Mbilinge Mbilinge za kutaka kuondoka FC Barcelona zilizodumu kwa zaidi ya majuma mawili yaliyopita, hatimae nahodha na mshambuliaji wa kikosi cha klabu hiyo Lionel Messi ameonekana katika viwanja vya mazoezi.
Messi alifika mazoezini baada ya kufanya tangazo la Jezi ya tatu kupitia mitandao ya kijamii ikiwa ni kujiandaa na msimu mpya wa Ligi ya Hispania (La Liga).
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Argentina, mwishoni mwa juma lililopita alithibitisha kuendelea kuitumikia klabu hiyo ya Cataluna, baada ya kuutingisha uongozi wa FC Barcelona kwa kutaka kuondoka na kwenda kwingine kusaka changamoto mpya ya soka lake.
Messi alikuwa akiamini vifungu katika mkataba wake vinamruhusu kuondoka kama mchezaji huru lakini kwa pamoja uongozi wa FC Barcelona na LaLiga walikataa madai hayo, na kusema yoyote atakaehitaji kumsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33, lazima alipe kiasi cha Euro milioni 700, kama ada yake ya uhamisho.
Mshindi huyo mara sita wa tuzo ya Ballon d’Or alimtuhumu rais wa klabu ya Barcelona Josep Maria Bartomeu kwa kueleza aliwahi kusema: “Messi atakuwa huru kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu 2019-20 endapo akihitaji.”
Kutokana na hali ya mvutano kutulia kwa kupatiana kwa muafaka wa pande zote mbili, Lionel Messi atakuwa sehemu ya kikosi cha meneja mpya wa FC Barcelona Ronald Koeman na amekua sehemu ya wachezaji wanaohudhuria mazoezi baada ya kufanya vipimo vya Corona juma lililopita.