Baada ya kuwepo taarifa za kutaka kurejea katika klabu yake ya zamani, aliyekuwa kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi amesema hana mpango wa kurudi tena Mbeya City ambayo aliipandisha daraja.

Kocha Mwambusi alitajwa kuwa miongoni mwa makocha wanne walioomba kufundisha timu hiyo, lakini amesisitiza kuwa hakuna ukweli wa jambo hilo kwa vile hana mpango huo kwani ameamua kupumzika kujihusisha na masuala ya soka kwa sasa

“Sina mpango huo, watu wametaja kuwa ningefundisha timu nyingi lakini nimeamua kupumzika kwa sasa hivyo hakuna ukweli wowote kwamba nimeomba kazi ya kuifundisha Mbeya City, sijafikiria hivyo kabisa, ” alisema Mwambusi.

Mapema mwezi Julai Juma Mwambusi aliachana na Yanga baada ya kuitumikia klabu hiyo  kwa misimu miwili na kuipa mafanikio makubwa ikiwemo kutwaa mataji mawili ya ligi ya Vodacom na kombe moja la FA.

Mbeya City kwa sasa inashika nafasi ya 7 katika msimamo wa ligi kuu ya Vodacom ‘VPL’ baada ya kucheza michezo minne.

Mwendesha Mashtaka Mkuu Kenya aigeukia Tume ya Uchaguzi
Video: Mapya ya Lissu, Rais aamuru mwanawe auawe