Benchi la ufundi la Young Africans lina matumaini makubwa ya kuendelea kufanya vizuri kwenye michezo ya Ligi Kuu, baada ya kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM kutoka visiwani Zanzibar jana Jumatano, jijini Dar es salaam.

Young Africans waliutumia mchezo huo uliomalizika kwa ushindi wa mabao mawili kwa sifuri, kama sehemu ya kujiandaa na mchezo wa mzunguuko watano wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam, Jumamosi Oktoba 03.

Kocha Msaidizi wa Young Africans Juma Mwambusi amesema kuwa wanaamini kwa maandalizi ambayo wanayafanya, watapata matokeo chanya kwenye michezo ijayo ya Ligi Kuu, wakianza na mchezo dhidi ya Coastal Union.

Amesema kuwa ana imani kwamba wachezaji wake watakuwa kwenye ubora kwa kadri ambavyo wanaendelea kutimiza majukumu yao ndani ya uwanja, pamoja na kucheza kwa kujituma.

“Sio kazi nyepesi kupata ushindi ndani ya uwanja, ila inahitaji maandalizi mazuri na makubwa. Tunachokifanya kwa sasa ni kuona tunakuwa na timu bora itakayotupa matokeo hivyo tutapambana mbele ya Coastal Union kupata ushindi.

“Timu nzuri ambayo tunakutana nayo hatuibezi tunawaheshimu wapinzani wetu lakini hamna namna tunahitaji ushindi na kupata pointi tatu, mashabiki wajitokeze kwa wingi,” amesema kocha huyo ambaye aliwahi kuinoa Mbyea City ya Mbeya.

Kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya KMKM uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, mabao ya Young Africans yalifungwa na kiungo kutoka DR Congo Mukoko Tonombe dakika ya 10 na 30.

Shibuda :Sera ya majimbo ni chanzo cha mifarakano
Datavision International yasherehekea miaka 22 ya mafanikio