Beki na Nahodha wa kikosi cha Young Africans Bakari Nondo Mwamnyeto amesema haikuwa rahisi kuifunga Simba SC Jumamosi (Mei 28), katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Young Africans iliibuka na ushindi wa 1-0, na kuivua rasmi ubingwa Simba SC wa Kombe la ‘ASFC’ ambao waliutetea kwa mara ya pili mfululizo mkoani Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika msimu uliopita.
Mwamnyeto amesema kupambana bila kuchoka huku wakifunga mipango na kuzima mbinu za wapinzani wao, ilikua kilelezo kikubwa kwao kuibuka kidedea katika mchezo huo ambao ulikua na vuta nikuvute hasa kipindi cha pili.
“Kocha alituhusia tupambane na kulinda bao tulilolipata kipindi cha kwanza, tukiwa katika vyumba vya kubadilishia wakati wa mapumziko, tulisisitizwa sana hilo kwa sababu tulifahamu tunaongoza na kama tungeshindwa kulinda lile bao, basi mambo yangekua magumu sana,”
“Tunamshukuru Mungu tulifanikiwa kwa mbinu ambazo kocha wetu alituelekeza tuzitumie katika kipindi cha pili, japo wengi waliamini Simba SC walicheza vizuri katika kipindi cha pili, lakini sisi tulijua tunafanya nini wakati ule.” Amesema Mwamnyeto
Young Africans itacheza Fainali ya ‘ASFC’ Julai Mbili dhidi ya Coastal Union ya Tanga ambayo imeitoa Azam FC katika mchezo wa Nusu Fainali uliochezwa jana Jumapili (Mei 29), katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kwa changamoto ya mikwaju ya penati 6-5.