Baadhi ya Wachezaji wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young African wameweka wazi kuwa watapambana kuhakikisha kikosi chao kinapata ushindi dhidi Marumo Gallants.
Young Africans itachuana na Marumo Gallants keshokutwa Jumatano (Mei 10) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, saa 10:00 jioni katika mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku mchezo wa Mkondo wa Pili ukipangwa kuchezwa Mei 17 Afrika Kusini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wachezaji hao wamekiri wapinzani wao wana kikosi kizuri, lakini watahakikisha ushindi unabakia nchini ili kujiweka katika mazingira mazuri kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili ambao utaamua nani atatinga Fainali, Kombe la Shirikisho.
Nahodha na Beki wa Young Africans Bakari Nondo Mwamnyeto, amesema kikosi chao kimejipanga vizuri kuhakikisha wanamaliza kazi katika uwanja wa nyumbani.
Mwamnyeto amesema kiu yao ni kuona timu yao inatinga Fainali ya michuano hiyo ya Afrika, hivyo wamejipanga vyema kufanya mambo makubwa.
“Najua mchezo utakuwa mgumu, kikubwa tunahitaji kupata ushindi katika mchezo huu muhimu,” amesema.
Naye Kiungo Mshambuliaji kutoka Ghana, Benard Morrison amesema wachezaji wote wameapa kupambana kwa jasho na damu ili wafikie malengo.
“Sisi kama wachezaji tuna morali ya kutosha kuhakikisha tunashinda mabao mengi ili tuweze kupata urahisi katika mchezo wa marudiano,” amesema.
Marumo Gallant ilifanikiwa kufika Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa ushindi wa jumla wa 2-1 dhidi ya Pyramid ya Misri, huku Young Africans ikiibamiza Rivers United ya Nigeria kwa ushindi wa jumla wa 2-0.