Beki na Nahodha wa Young Africans Bakari Nondo Mwamnyeto ameonesha ujasiri kuelekea mchezo wa Kwanza wa Kundi C, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Young Africans itacheza ugenini Tunisia Jumapili (Februari 12) majira ya saa moja usiku kwa saa za Tanzania, dhidi ya US Monastir ambayo imedhamiria kushinda nyumbani katika Uwanja wa Hammadi Agrebi, mjini Tunis.

Mwamnyeto amesema baada ya kuwasili Tunisia, wachezaji wote wa Young Africans wapo katika hali nzuri, na kila mmoja ana ari kubwa ya kupambana ili kuipa matokeo chanya timu hiyo.

Amesema anatambua mchezo utakua mgumu kutokana na mazingira ya soka la Afrika, ambayo siku zote yamekua yakiipa nafasi kubwa timu mwenyeji, lakini wao wamejipanga kuondoka na furaha siku ya Jumapili.

“Nia yetu ni moja tu tukiwa huku Tunisia, nayo ni kupata matokeo mazuri tukiwa ugenini, tunafahamu jinsi gani ilivyokuwa ngumu kupata matokeo mazuri ugenini,”

“Tutapambana kwa ajili ya kuhakikisha tunafanikisha jambo letu, ili tuanze vyema kuvuka hatua ya makundi.” amesema Mwamnyeto

Kikosi cha Young Africans kinatarajia kuanza mazoezi nchini Tunisia leo Alhamis (Februari 09), chini ya Kocha Nabi, huku wakiamini muda wa kufanya hivyo utatosha kabla ya kuingia dimbani Jumapili kuikabili US Monastir.

Fiston Mayele anaitaka GAME na US Monastir
Nasreddine Nabi: Tuna kazi kubwa Tunisia