Jeshi la Polisi limemuachia kwa dhamana, Mtume na Nabii, Boniface Mwamposa baada ya kukamilisha kumhoji kufuatia tukio la watu 20 kupoteza maisha kwa kukanyagana kwenye mkutano wake wa injili, ikielezwa kuwa walikuwa wanawania kukanyaga mafuta ya upako, Mkoani Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, David Miseme amesema kuwa Mwamposa na wenzake saba wameachiwa baada ya kuhojiwa kwa kina na jeshi hilo kupata taarifa walizokuwa wanazihitaji kwa ajili ya uchunguzi.
Alieleza kuwa watuhumiwa hao nane kwa pamoja wanatakiwa kuwa wanaripoti katika kituo cha polisi wakati uchunguzi ukiendelea.
“Watuhumiwa wanane waliokamatwa akiwemo Mwamposa, walihojiwa kwa kina na baada ya kujiridhisha na kupata yale yaliyokuwa yanahitajika katika uchunguzi waliachiwa kwa dhamana kwa mujibu wa sheria, na watakuwa wakiripoti wakati uchunguzi ukiendelea,” Mwananchi linamkariri Kamanda Miseme.
Katika hatua nyingine, Kamanda Miseme alieleza kuwa kufuatia tukio hilo, Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro alituma timu ya wataalam wa uchunguzi wa sayansi ya jinai ili wasaidiane na askari wengine wa mkoa wa Kilimanjaro.
Tukio hilo lililosababisha pia majeruhi 16, lilizua taharuki na mshtuko huku Mkuu wa Mkoa huo, Anna Mghwira akiwataka wananchi kuchukua tahadhari wanapokuwa wanafuata masuala ya kiimani.
Rais John Magufuli alituma salamu za rambirambi na pole kwa waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki na kwa Watanzania wote. Pia, aliagiza shughuli zote za kiimani na kidini zisizuiwe bali makosa ya kibinadamu yafanyiwe kazi.