Klabu ya Simba imelalamika kunyimwa penati mbili na mwamuzi Heri Sasii katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi Young Africans, uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja mwishoni mwa juma lililopita.

Simba imewasilisha malalamiko hayo kupitia idara yake ya habari na mawasiliano inayoongozwa na Haji Sunday Manara katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo mchana makao makuu ya klabu hiyo yaliopo mtaa wa Msimbazi jijini Dar es salaam.

Manara ametumia picha za video kuonyesha namna walivyonyimwa penati hizo mbili na mwamuzi Sasii, ambaye alionekana katika picha hizo akiwa karibu na matukio ambayo yaliwahusisha wachezaji wa Young Africans Calvin Yondan Mbuyi na Papy Kabamba Tshitshimbi kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Manara aliwabeza watani wao hao wa jadi, kwamba ni kawaida yao kupendelewa na marefa kila wanapokutana na Simba amesema watapeleka malalamiko Bodi ya Ligi dhidi ya refa huyo na wengine walioionea timu yao katika mechi zilizotangulia.

Akasema huo ni mwendelezo wa matukio ya klabu yake kutotendewa haki na marefa katika mechi za Ligi Kuu msimu huu, akidai walinyimwa pia penalti mbili katika mechi dhidi ya Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, kabla ya wapinzani wao wengine, Singida United kupewa penalti ya utata Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga.

Simba ilitoa sare ya 2-2 na Mbao FC kabla ya kushinda 3-1 dhidi ya Stand United, katika mchezo ambao pia walikataliwa bao zuri la mshambuliaji wao, Laudit Mavugo.

Pamoja na hayo, Manara amelalamikia kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kukataa ombi la klabu, Simba na Yanga kutaka mchezo wao ufanyike Uwanja mkubwa wa Taifa na kuupeleka Uwanja mdogo wa Uhuru.

Manara amesema hali hiyo ilizikosesha klabu fedha kutokana na watazamaji kutojitokeza kwa wingi kwa kuhofia usalama wao kutokana na udogo wa Uwanja wa Uhuru.

Aidha, Manara mtoto wa mchezaji wa zamani wa Yanga, Sunday Manara ‘Kompyuta’ amesema kwamba kikosi cha Simba sasa kinaelekeza nguvu zake katika mchezo wake ujao dhidi ya Mbeya City Jumapili Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Amesema kwamba kikosi kitaondoka Jijini Ijumaa kwenda Mbeya, ambako kitakaa kwa muda mrefu kutokana na kukabiliwa na mechi nyingine pia za Ligi Kuu Nyanda za Juu Kusini. Amesema hakuna majeruhi mpya kikosini, ukiondoka kipa Said Mohammed ‘Nduda’ na mabeki Shomary Kapombe na Salim Mbonde.

RC Rukwa awataka watumishi wa umma kutobweteka
Video: Huu si wakati wa kutupiana lawama- Mrisho Mpoto