Mwanafunzi Anna Zambi aliyepoteza familia yake katika ajali ya gari na kupelekea kifo cha baba, mama na wadogo zake watatu wakati wakienda kwenye mahafali yake mkoani Tanga mwaka 2019 amefaulu mitihani yake kwa kupata daraja la pili (Division II) katika matokeo yake ya kidato cha nne yaliyotolewa jana.
Anna Zambi amemaliza elimu yake ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Mather Theresia of Calcuta iliyopo mkoani Kilimanjaro .
Wazazi wa Anna walikuwa wakifahamika kwa majina ya Lingston Zambi na Winifrida Lyimo na wadogo zake watatu, Lulu, Andrew na Grace waliaga dunia katika ajali ya gari walilokuwa wamepanda kusombwa na maji, kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha wilayani Handeni mkoani Tanga.
Waziri jinsia wazee na watoto Ummy Mwalimu aliandika kupitia ukurasa wake wa tweeter “hili jambo ni kubwa mno kwa mtoto Anna Zambi, inaumiza sana ninamuombea kwa Mungu ampe nguvu na moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu, kama mzazi na Waziri mwenye dhamana ya Ustawi na Maendeleo ya Watoto nami nitamfikia Anna kwa ajili ya kumfariji na ‘support’ nyingine.” alisema Waziri Ummy.
Aidha taarifa za msiba huo kwa Anna zilitolewa mara baada ya kumaliza mitihani yake ya Taifa, watu mbalimbali mashuhuri waliguswa na msiba huo mzito akiwemo Mbunge wa Bumbuli, January Makamba na wengi walijitolea kumsaidia binti hiyo akiwemo Zamaradi Mketema.
Ilikuwa pigo kubwa kwa Anna na watanzania kwa ujumla, ni msiba mzito kwa binti huyo mdogo lakini uzuri Mungu ametuumbia kusahau sasa Anna anaishi na shangazi yake mjini Arusha.