Mwanafunzi Mwita Juma mwenye umri wa miaka 19 wilayani Butiama mkoani Mara amefikishwa katika Mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Musoma akikabiliwa na kosa la kumjeruhi kwa panga Mwalimu wake Majogoro John kinyume na kifungu cha sheria namba 222 (a) cha kanuni ya adhabu kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Akisoma hati ya mashitaka wakili wa serikali Mwanadamizi Valence Mayenga mbele ya hakimu Tumaini Marwa katika kesi namba 13 ya mwaka 2020 amesema mnamo tarehe 22 mwezi Septemba 2020 mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo akiwa eneo la shule ya Sekondari ya Kiagata kwa kumkata kwa panga Mwalimu Majogoro John pale mwalimu huyo alipomwamuru akalete wazazi wake.

Mara baada ya mtuhumiwa huyo kusomewa shitaka, hakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na hakimu Tumaini Marwa amesema uchunguzi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe 12 Mwezi Oktoba 2020 kesi hiyo itakapo tajwa tena mahakamani hapo.

Hakimu Marwa amesema dhamana ya mshitakiwa ipo wazi na mshitakiwa anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja ambapo masharti ya dhamana ni shilingi milioni 10, mali isiyo hamishika iwe na hati ya umiliki na mdhamini aambatanishe na barua ya utambulisho kutoka makazi anayokaa.

Mshitakiwa alikosa mdhamini na kupelekwa rumande hadi pale kesi hiyo itakapotajwa tena.

HESLB yatoa siku 5 waliohitimu JKT kuomba mikopo
Wanaowarubuni wapiga kura wapewa onyo