Jeshi la polisi nchini Kenya linamshikilia mwanafunzi wa kiume wa kidato cha tatu anayedaiwa kumuua kwa kipigo baba yake mzazi mwenye umri wa miaka 50, baada ya kugundua kuwa aliuza jogoo wake bila ruhusa yake.  

Ripoti ya jeshi la polisi imeeleza kuwa tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Barotion, Kaunti ya Kericho. Mwenyekiti wa kijiji hicho, Sarah Sigey ameviambia vyombo vya habari kuwa baba na mwana waliingia kwenye mgogoro baada ya mwana kufika nyumbani na kubaini kuwa baba ameuza jogoo wake.

“Mvulana huyo alihoji kwa jazba na baba yake naye akamjibu kwa ukali kama mtoto, ndipo mvulana huyo akamvamia kuanza kupigana naye,” alisema Sigey.

Alieleza kuwa mashuhuda wa tukio wanasimulia kuwa mvulana huyo alishika rungu na kumpiga baba yake mara kadhaa kichwani.

Majirani waliposikia sauti za yowe na kuomba msaada, walifika haraka eneo la tukio na kumkuta mzee huyo akiwa hajitambui. Imeelezwa kuwa walimkimbiza katika hospitali ya Londiani, lakini alifariki wakati akipatiwa matibabu.

Polisi wameeleza kuwa baada ya kufanya mauaji hayo, mvulana huyo alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Londiani ambapo anashikiliwa.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya Mtakatifu Joseph kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na kuhifadhiwa.

Kauli ya Mbunge Tabasamu yaibua minong’ono mkutano wa Samia, vijana
Serikali yaja na mkakati wa kumlinda Mzee