Mfanyabiashara Robert Mwikwabe, maarufu kama Ndugu, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumpiga risasi ya kichwani na kusababishia kifo papo hapo mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya sekondari Sirari, Masaite Mrimi(17).
Tukio hilo lilitokea eneo jirani na nyumbani kwa marehemu , ambako kulitokea mzozo kati ya Robert na wazazi wa mwanafunzi huyo. Kufuatia mzozo huo, mwanafunzi huyo aliyekuwa na panga mkononi, alimtishia kumkata Robert, ambaye alichomoa silaha yake aina ya bastola na kumpiga risasi kichwani na kumsababisha kifo.
Baada ya tukio hilo, familia ya marehemu na wananchi walianza kumfukuza Robert aliyeacha lori lake likiwa na mawe na kukimbilia lori lake lingine la jirani. Kisha alikimbilia Kituo cha Polisi Sirari, kuokoa maisha yake.
Kutokana na tukio hilo, Mwikwabe ambaye pia ni mmliki Hoteli katika mji mdogo wa Sirari wilayani Tarime mkoani Mara, alinusurika kuteketezwa yeye na familia yake, hali hiyo ilitokea baada ya wananchi kuamua kuchoma moto lori la mfanyabiashara huyo na kwenda nyumbani kutaka kuchoma hoteli na nyumba.
Lakini, polisi na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorius Luoga walifanya juhudi kubwa kuwazuia wananchi hasa vijana, kuacha kuteketeza mali za mfanyabiashara huyo yakiwemo magari, ambayo sasa yamehifadhiwa kituo cha polisi kwa ajili ya usalama.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Tarime-Rorya, Andrew Satta alithibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo na kwamba maiti imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya Tarime.