Siku chache baada ya kuripotiwa tukio la kuuawa kwa aliyekuwa mwanakwaya wa kanisa la AICT Chang’ombe, Mariam Charles, ndugu wa marehemu huyo wameeleza kupata ujumbe wa vitisho kutoka kwa mtu anayejieleza kuwa ndiye muuaji.

Dada wa marehemu, Lucy Enock ameeleza kuwa amekuwa akipokea ujumbe mfupi wa simu kupitia simu ya Mariam ambayo mtu huyo anaitumia.

Alisema hivi karibuni mtu huyo amemuandikia ujumbe unaosomeka, “nimemuua Mariam kwa sababu ya uongo wake kwangu na alinitengenezea njama kwa mama (anamtaja) ili nikamatwe, nikagundua baada ya mama huyo kumpigia akiwa anaoga”

Lucy anakaririwa na Mwananchi akieleza pia kuwa kuna jumbe nyingine za vitisho na nyingine ambazo mtu huyo amedai kuwa ameshindwa kujiua au kukimbia na badala yake ameamua kujisalimisha polisi.

“Jamani kama kukimbia ningeweza, maana nilikuwa nimefika nje ya mji, saa hivi nimerudi naenda polisi mwenyewe, hata kujiua nashindwa hata nikijaribu kwa sababu sijaua kwa kukusudia,” Lucy aliusoma ujumbe huo. “Ni bora kuuliwa kuliko mateso ya nafsi ya Mariam ninayoyapata. Mariam ananitokea kila nikitaka kujiua..” Mwananchi wanamkariri tena Lucy akisoma ujumbe wa mtu huyo.

Mariam alikutwa akiwa amefariki katika nyumba ya wageni iliyoko Boko jijini Dar es Salaam, na anadaiwa kuwa alikuwa na mchumba wake ambaye pia ni mwanakwaya.

Mama wa Mariam alieleza kuwa mwanaye alimuaga anaenda kukuta na na mchumba wake na kwamba tarehe ya kutolewa mahari ilikuwa jana. Lakini Septemba 4 alipokea ujumbe ukieleza kuwa “tayari nimeisha muua mwanao”.

Anasema baada ya kuupata ujumbe huo, kwa mshtuko mkubwa walienda kuripoti polisi na baada ya msako mwanaye alikutwa akiwa amekufa.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa jeshi hilo linaendelea kuchunguza tukio hilo.

Video: Jerry Muro aichana hotuba aliyoandaliwa, asema ni upuuzi
Anayedaiwa kumpa mke wa Mugabe PhD feki akwama