Mwanamke wa Kivietnam aliyekuwa anashikiliwa gerezani kwa zaidi ya miaka miwili kwa tuhuma za kupanga kumuua Kim Jong Nam ambaye ni kaka yake Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, ameachiwa huru.
Doan Thi Huong mwenye umri wa miaka 30 alikuwawa anashikiliwa gerezani nchini Malaysia. Alihukumiwa pamoja na mwanamke mmoja wa Indonesia ambao kwa pamoja walidaiwa kumwangia usoni Kim Jong Nam kimiminika ambacho kinatambulika kama silaha ya kikemikali. Kim ambaye ni kaka yake kiongozi wa Korea Kaskazini alipoteza maisha kutokana na tukio hilo.
Wawili hao walidaiwa kutenda kosa hilo Februari 2017 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kuala Lumpur.
Wanawake hao walikana kutenda makosa hayo wakieleza kuwa walichanganywa kwa kupewa maji ambayo walidhani wanafanya utani kwa ajili ya kipindi cha runinga, na kwamba hawakufahamu kuwa ni kemikali yenye sumu.
Waliiambia Mahakama kuwa wao ni watu wasio na hatia ambao waliingizwa kimtego kwenye njama ya mauaji ya Kim Jong Nam.
Huong alifungwa miaka kadhaa jela lakini miaka hiyo imepunguzwa kutokana na namna alivyokuwa akiishi ndani ya gereza hilo. Mwezi uliopita alikiri kufanya kosa la kusambabisha majeraha dhidi ya Kim Jong Nam.
Huong anatarajiwa kurejea nchini kwao Vietnam mapema leo.
“Nilikutana na Doan jana alipokuwa gerezani na nikampa nguo mpya pampja na viatu. Alikuwa na furaha kuu ya kuachiwa huru na anasubiri kwa hamu kuungana tena na familia yake,” alisema Hisyam Teh Poh Teik ambaye ni mwanasheria wa mwanamke huyo.