Mahakama jijini Ljubljana nchini Slovenia imemhukumu kifungo cha miaka miwili jela, mwanamke aliyejikata mkono wake wa kushoto akitarajia kulipwa zaidi ya £925,000 kama fidia ya matibabu kupitia mashirika ya bima.

Julija Adlesic mwenye umri wa miaka 22, alibainika kuwa akipanga na mpenzi wake kuukata mkono wake kwa makusudi wakiwa nyumbani kwao katika jiji hilo, mapema mwaka 2019.

Baada ya uchunguzi wa kina, Adlesic alikutwa na hatia ya kujaribu kufanya udanganyifu ili kujipatia fedha kwenye mashirika ya bima. Alikata bima za afya kwenye mashirika kadhaa mwaka mmoja kabla.

Kwa mujibu wa sheria za bima, endapo tukio hilo la kukata mkono lingeonekana ni halisi, angelipwa nusu ya kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya matibu punde tu baada ya kuripoti tukio, na kiasi kingine kingeendelea kulipwa.

Aidha, Mahakama hiyo haikumuacha salama mpenzi wake na baba wa kijana huyo, ambao walibainika kushiriki moja kwa moja katika kupanga njama. Hivyo, kijana huyo alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na baba yake kifungo cha nje.

Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, mpenzi wa mwanamke huyo aliingia kwenye mitandao na kutafuta mkono usio halisi unavyoweza kufanya kazi, siku moja kabla ya tukio hilo. Hivyo, hiyo ilionesha kuwa kitendo hicho kilipangwa makusudi.

Imeelezwa kuwa wawili hao (kijana na baba yake) walimpeleka hospitalini wakieleza kuwa amejikata mkono wakati akikata matawi ya mti, lakini waliacha nyumbani kwao kipande cha mkono uliokatwa badala ya kuupeleka pia hospitalini.

Alipopewa nafasi ya kujitetea mahakamani, Adlesic alisisitiza kuwa hakuwa na hatia kwani hakuna mtu anayeweza kujikata kabisa mkono wake kwa makusudi.

“Hakuna mtu anayependa kuwa kilema. Ujana wangu umeharibika. Nimepoteza mkono wangu nikiwa na miaka 21. Ni mimi pekee ninayefahamu ilikuwaje,” alisema Adlesic.

Jaji Marjeta Dvornik aliendelea na msimamo wa Mahakama, akieleza kuwa wanaamini hukumu hiyo imetenda haki na iko sahihi.

Mwalimu: Tutalipa watumishi wa serikali fidia
Baada ya CCM jana, ACT Wazalendo kukiwasha leo Zanzibar