Mahakama ya juu zaidi nchni Ufaransa imeridhia uamuzi wa kumnyima hati ya kusafiria pamoja na kukataa maombi ya uraia ya mwanamke wa Algeria aliyeolewa na raia wa Ufaransa, kwa kukataa kushikana mikono na viongozi wa nchi hiyo kwa sababu alizodai ni za imani ya dini yake.
Mwanamke huyo mwenye imani ya dini ya Kiislamu alijitetea kuwa imani yake hairuhusu mwanamke kushikana mikono na afisa mwandamizi pamoja na wanasiasa wakati wa hafla ya kukabidhiana uraia, kusini mashariki mwa Isere. Tukio hilo lilitokea Juni 2016.
Serikali ya Ufaransa ilieleza kuwa tabia aliyoionesha mwanamke huyo haiendani na utamaduni wa jamii ya nchi hiyo, hivyo hastahili kupewa uraia kwa lengol a kujiunga na jamii asiyoendana nayo.
Mwanamke huyo ambaye alifunga ndoa na raia wa Ufaransa mwaka 2010, alikata rufaa kwenye mahakama hiyo ya juu Aprili 2017 akiwatuhumu maafisa wa Ufaransa kwa matumizi mabaya ya madaraka.
Mahakama ya juu zaidi aliyokatia rufaa imesisitiza kuwa maafisa wa Serikali hawakufanya jambo lolote linalovunja sheria za nchi hiyo dhidi ya haki ya mwanamke huyo.