Mwanamke wa kwanza Duniani amefanikiwa kuponywa na ugonjwa wa Ukimwi kwa kupandikizwa seli shina katika mwili wake ambaye alikuwa anaugua saratani ya damu.
Mwanamke huyo alipandikizwa seli hiyo kutoka kwa mfadhili ambaye kwa asili alikuwa sugu kwa virusi vinavyosababisha Ukimwi lakini tangu apandikizwe seli hiyo, mwanamke huyo hakupata VVU kwa muda wa miezi 14.
Kesi hiyo, iliyowasilishwa na wanasayansi februari 16, 2022 katika Kongamano la Virusi vya Ukimwi na Maambukizi mjini Denver, Marekani, ilikuwa ya kwanza kuhusisha damu ya kitovu kutibu saratani ya damu ambayo ni mbinu mpya zaidi inayoweza kufanya matibabu kupatikana kwa watu wengi zaidi.
“Hii sasa ni ripoti ya tatu ya tiba katika mazingira haya, na ya kwanza kwa mwanamke anayeishi na VVU,” alisema Sharon Lewin, Rais Mteule wa Jumuiya ya Kimataifa ya UKIMWI.
Taarifa za awali za visa vya kuponywa UKIMWI zilitokea kwa wanaume, mmoja mwenye asili ya mzungu na mwingine Latini ambao walikuwa wamepokea seli shina za watu wazima, ambazo hutumiwa mara kwa mara katika upandikizaji wa uboho.
Kesi hiyo ilikuwa sehemu ya uchunguzi mkubwa wa Marekani wa watu wanaoishi na VVU ambao walikuwa wamepokea aina moja ya kupandikiza damu kutibu saratani na magonjwa mengine sugu.
Mtu wa kwanza kutibiwa virusi vya ukimwi ni Timothy Ray Brown ambaye alifariki kutokana na saratani lakini alipandikizwa uboho kutoka kwa mtu ambaye alikuwa na kinga dhidi ya VVU mwaka2017.
Hii ilimaanisha kwamba alikuwa hahitaji tena dawa za kukabiliana na virusi vya ukimwi hivyo basi alisalia bila maambukizi yoyote ya virusi hivyo vinavyosababisha ukimwi kwa maisha yake yote mpaka anafariki dunia.
Kisa cha pili cha kuonekana kupona kwa VVU ni cha Mwanamke kutoka nchini Argentina ambaye alionekana kupona kutokana na virusi vya ukimwi bila ya kutumia madawa au kupata matibabu ambapo madaktari wanaamini kuwa mfumo wa kinga ya mwili wa mgonjwa huyo ulisafisha kirusi hicho baada ya vipimo kwa zaidi ya seli zake bilioni moja viligundua kuwa hakukuwa na dalili zozote za maambukizi.
Shirika la kimataifa kuhusu wagonjwa wa ukimwi duniani limesema kwamba Iwapo mfumo huu utatumiwa unaweza kugundua njia ya kumaliza au kutibu VVU ulimwengu kwa kuwa visa hivi vinatoa matumaini kwamba dawa ya kutibu ukimwi inaweza kupatikana.