Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr ambaye mmoja wa washirika wakubwa wa Rais, Donald Trump, amejiuzulu.
Barr anajiuzulu wakati kukiwa na mvutano wa muda mrefu na rais juu ya madai yasiyo na msingi ya rais ya wizi wa kura katika uchaguzi mkuu uliomalizika na uchunguzi juu ya mtoto wa rais mteule, Joe Biden.
Jana Jumatatu, Barr alikwenda Ikulu ya Marekani White House, ambapo Trump alisema mwanasheria mkuu huyo aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu.
Trump ameonyesha hasira yake hadharani juu ya taarifa ya Barr aliyoitoa kwa shirika la habari la Associated Press mapema mwezi huu kwamba Idara ya Sheria haikuona udanganyifu mkubwa wa uchaguzi ambao ungebadilisha matokeo ya uchaguzi huo.
Trump amesema Naibu Mwanasheria Mkuu, Jeff Rosen atakuwa Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.