Katika hali isiyo ya kawaida mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 29 Muhammad Malik, ameibua mjadala kote mitandaoni baada ya kueneza picha yake kwenye mabango makubwa kadhaa kote Birmingham na kutangaza katika tovuti yake maalum ‘findmalikawife.com’ aliyoitengeneza ili kutafuta mwenzi mtarajiwa wa maisha yake.
Kwa mujibu wa Birmingham Live Malik alisema hapingani na wazo la kupangiwa ndoa kutokana na utamaduni wao lakini anataka kujaribu kupata mtu kwa jitihada zake binafsi kwanza.
“Bado sijapata msichana anayefaa, ni ngumu huko nje lakini ilinibidi nitumie mabango ili nionekane!” alisema kwenye tovuti yake.
Wengi wamekuwa wakijiuliza kwanini mwanaume huyo ameshindwa kutumia njia ambazo zinatumiwa na wanaume wengine pindi wanapokuwa wanatafuta wachumba kwa ajili ya ndoa.
Akiendelea kuweka bayana kilichompelekea kuanzisha kampeni hiyo ya kutafuta mke kwa njia ya kujitangaza kwenye mabango Malik alisema.
“Kwa kweli, kuna tafiti nyingi zinazoonyesha kuwa ndoa za kupanga zina faida nyingi. Lakini kwa sasa nahitaji tu kujaribu kutafuta mtu peke yangu kwanza.”
“Mpenzi wangu anapaswa kuwa mwanamke wa kiislamu mwenye umri wa miaka 20, ambaye anajitahidi kuzingatia dini yake,”
“Naruhusu kabila lolote lakini nina familia yenye kelele ya Kipunjabi, kwa hivyo utahitaji uvumilivu pia.”
Malik alianza kuyaeneza mabango hayo mapema januari 1, 2022. Huku mapokezi ya taarifa za yeye kutafuta mke yakiwa makubwa kiasi cha kutiririsha mamia ya jumbe kutoka kwa wanawake mbali mbali.
“Bado sijapata muda wa kusoma ujumbe mmoja baada ya mwingine ili kujua hatma ya ninachokitafuta,” aliiambia shirika la BBC.