Mwanaume mwenye umri wa miaka 76 anayeaminika kuwa ndiye mkuu wa familia kubwa zaidi duniani inayoishi pamoja, amefariki dunia jana, Juni 13, 2021.

Ziona Chana, aliyeishi katika jimbo la Mizoram liliko nchini India alikuwa na wanafamilia wasiopungua 181. Chana ameacha wajane 39, watoto 94 na wajukuu 33 na vitukuu kadhaa.

Waziri wa Mizoram, Zoramthanga amethibitisha kutokea kwa kifo cha Chana kupitia akaunti yake ya Twitter akitoa salamu zake za rambirambi.

Kwa mujibu wa ripoti za kitabibu zilizotolewa na Serikali ya Mizoram, Chana alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kisukari. Imeelezwa kuwa afya yake ilizorota akiwa amejilaza nyumbani kwake, katika kijiji cha Baktawng Tlangnuam.

PTI News limeripoti kuwa mwanaume huyo alipozidiwa alikimbizwa hospitalini, lakini alipofika madaktari walibaini amekwishapoteza maisha.

Hata hivyo, bado kuna ugumu katika kuthibitisha kuwa ndiye mwanaume mwenye familia kubwa zaidi duniani kwakuwa wapo baadhi ya watu ambao wanadai kumzidi idadi ya wanafamilia, ingawa wao pia hawajathibitishwa.

Maisha ya Chana na familia yake yalikuwa sehemu ya vivutio vya kitalii katika eneo hilo. Familia hiyo iliishi pamoja katika nyumba iliyoitwa ‘Chuuar Than Run’ kwa maana ‘nyumba ya kizazi kipya’. Nyumba hiyo ina vyumba 100. Vyombo vya habari vya eneo hilo vimeeleza kuwa wake zake wanakaa kwenye bweni moja ambalo liko karibu na chumba cha kulala cha mume wao.  

Je, unamfahamu mwanaume anayeishi mwenye wake na watoto wengi zaidi ya Chana? Unaweza kusaidia kuweka rekodi sawa. Andika ‘comment’ yako hapo chini.

Musukuma: Faini ya 10,000 ni nyingi tungeweka hata 2000
Mkuu wa Twitter aweka bendera ya Nigeria mtandaoni