Mwandishi wa habari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, aliyepotea kwa siku tatu amekutwa akiwa katika hali mbaya na dhaifu, kwa mujibu wa taarifa za muajiri wake.

Kituo cha redio cha Svein ambacho ni muajiri wa mwandishi huyo ajulikanaye kwa jina la Hassan Murhabazi, kimeeleza jana jioni kuwa alikutwa katika jiji la Bukavu siku hiyo na alisema alikuwa ametekwa.

“Yuko katika hali mbaya na dhaifu lakini amethibitisha kuwa alikuwa ametekwa. Sababu za kutekwa bado hazijawa wazi na tutatoa taarifa rasmi baada ya kufanyiwa vipimo vya afya,” taarifa ya kituo hicho imeeleza.

Matukio ya utekaji yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika eneo la jimbo la Kivu ambalo liko ndani ya jiji la Bukavu.

Kwa mujibu wa shirika la Waandishi Wasio na Mipaka (RSF), Murhabazi alipotea baada ya kuondoka nyumbani kwake Jumanne, alipopigiwa simu na mtu asiyejulikana. Lakini katika hali ya kushangaza, simu yake ilikutwa nyumbani kwake.

Shirika hilo limeeleza kuwa alipokea ujumbe mfupi wa simu siku moja kabla ya tukio hilo ambapo ujumbe huo ulimuonya kutomzungumzia mgombea urais wa chama tawala.

Kwa mujibu wa RSF, nchi hiyo inashika nafasi ya 154 kati ya nchi 180 zilizofanyiwa utafiti kuhusu uhuru wa vyombo vya habari.

Bondia Mwakinyo ampiga chini Mayweather, amuomba kitu Rais
Video: Majaliwa ampongeza Mwakinyo kwa kumchapa Mwingereza Sam Egginton