Mshindi wa tuzo ya kimataifa ya umahiri wa uandishi wa habari nchini Mexico, Javier Valdez ameuawa kwa kupigwa risasi katika jimbo la Sinaloa.
Mwandishi huyo alifyatuliwa risasi na mtu asiyejulikana wakati alipokuwa katika gari lake akiendelea na shughuli zake za kila siku.
Valdez aliyekuwa na umri wa miaka 50, alishinda tuzo ya kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari iliyotolewa na Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) mwaka 2011, ambapo kazi yake ya namna alivyoripoti kwa umahiri kuhusu biashara ya dawa za kulevya ndiyo iliyompa heshima zaidi.
Vitendo vya mauaji ya waandishi wa habari vinavyofanywa na vikundi vya wafanyabiashara wa dawa za kulevya vimeendelea kukithiri nchini humo. Valdez ametajwa kuwa mwandishi wa tano kuuawa ndani ya mwaka huu.
Katika kitabu chake alichokichapisha mwaka jana, Valdez alieleza jinsi ambavyo maisha ya waandishi wa habari yako hatarini nchini humo dhidi ya makundi ya wauza dawa za kulevya.
“Kuwa mwandishi wa habari ni sawa na kuwa kwenye orodha mbaya. Hata kama una vizuia risasi (bullet proof) na walinzi, majambazi wataamua ni siku gani watakuua,” yanasomeka maandishi ya kitabu cha Valdez.
Valdez amekuwa akiandika vitabu vingi kuhusu biashara ya dawa za kulevya na matukio mengine ya kihalifu nchini Mexico. Kundi la wafanyabiashara za dawa za kulevya la Sinaloa linatajwa kuwa ndilo linalohusika na takribani 25% ya dawa za kulevya zinazoingia nchini Marekani. Kundi hilo lilikuwa linaongozwa na bilionea ‘El Chapo’ ambaye alikamatwa mwaka 2014 na yuko jela nchini Marekani akisubiri uamuzi wa mahakama dhidi ya mashtaka yanayomkabili.