Uongozi wa Halmashauri zote mkoani Tabora umetakiwa kuchagua vipaumbele vichache vya miradi itakayoanza nayo kuitekeleza ili iweze kutekelezwa kwa kiwango cha juu na ufanisi, hivyo kuwa na tija ambayo itawanufaisha wananchi wengi badala ya kunufaisha wachache.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya Madiwani wa Halmashauri ya Kaliua na Wakuu wa Idara yanayoendeshwa na wakufunzi kutoka chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo.

Amesema kuwa ni vyema madiwani kwa umoja wao wakakaa pamoja na kuangalia miradi michache ambayo inaweza kunufaisha Kata nyingi au wananchi na kuachana na ubinafsi ambao kila Diwani anataka mradi uanzie kwake na kujikuta wakichelewa kutoa maamuzi.

Aidha, amesema kuwa ubifsi huo unasababisha mara nyingi miradi kutekelezwa nusu nusu na hivyo kutokuwa msaada wa kuwaletea wananchi maendeleo ambayo wamekuwa wakiyatarajia.

“Miradi mingi inafanyika kwa kitu kinachoitwa kipaumbele, kila Diwani anavutia kwake katika mradi ambao ungejengwa katika Kata moja na kunufaisha wengi, ujue hawa wananchi watachelewa kupata maendeleo, ni vyema wakawa kitu kimoja katika kuchagua vipaumbele,”amesema Mwanri.

 

Hata hivyo, kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kaliua John Pima alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Madiwani na Wakuu wa Idara watoe maamuzi mazuri ambayo yatasaidia kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.

 

Anthony Joshua amtwanga Carlos Takam
RC Tabora ataka kuanzishwa kozi ya uhifadhi mazingira