Beki wa Azam FC, David Issa Mwantika amesema hataendelea kuitumiia klabu hiyo yenye maskani yake makuu Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam, baada ya kuitumikia kwa misimu minane.
Mwantia alijiunga na Azam FC mwaka 2012, lakini amekua na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza hasa msimu wa 2019/20 uliofikia tamati Julai 26.
Maamuzi ya beki huyo ya kuondoka Azam FC, yamekuja kufuatia mkataba wake kusaliwa na muda wa miezi mitano, na tayari maeshauarifu uongozi kuwa hatosaini mkataba mpya.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa, uongozi wa Azam FC uliua umeshaonyesha nia ya kutaka kuendelea na beki huyo, kwakuanza mazungumzo ya kumsainisha mkataba mpya.
“Ijumaa nilizungumza na viongozi ambapo walionyesha nia ya kutaka kunipa mkataba mpya, lakini nimewaomba waniache ili nikatafute changamoto mpya, mkataba wangu na Azam FC umebaki miezi mitano.
“Hivyo tumekubaliana kwa nia moja kuwa niwe mchezaji huru kuanzia sasa kuzungumza na timu yoyote na kucheza sehemu yoyote nitakayopata timu, iwe ndani ama nje ya nchi,” amesema Mwantika
Akizungumzia maisha ndani ya Azam FC, Mwantika alisema: “Nimecheza misimu minane, lakini ndani ya misimu hiyo ni mitano pekee ambayo nimeitumikia na nimecheza soka la uhakika kutokana na mambo mbalimbali yaliyokuwa yanajitokeza juu yangu kwenye timu.”
Mara kadhaa Mwantika alikuwa akikumbana na sakata la kutolewa kwa mkopo na timu yake, lakini alikuwa akigomea mpango huo ambapo msimu huu wakati wa dirisha dogo alitaka apelekwe Lipuli FC ya Iringa ambayo imeshuka daraja.