Mwamuzi Amin Mohamed Omar kutoka nchini Misri ametajwa kuwa Mwamuzi atakayechezesha mchezo wa Pili wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kati ya Horoya AC (Guinea) dhidi ya Simba SC (Tanzania).
Mpambano huo umepangwa kuchezwa Jumamosi (Februari 11) saa kumi jioni kwa saa za Tanzania, huku Simba SC ikitarajiwa kucheza kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa General Lansana Conté, mjini Conakry.
Rekodi za Mwamuzi Amin zinaonesha katika michezo 10 aliyochezesha ya mashindano ya CAF ngazi ya vilabu, ametoa jumla ya kadi 34 zikiwa ni wastani wa kadi 3.4 kwa mchezo, ambapo kati ya hizo, 33 ni za njano na moja ni nyekundu.
Katika michezo hiyo 10 aliyochezesha, ni mara moja tu timu iliyokuwa Ugenini ilipata ushindi ambayo ni JS Kabylie ya Algeria ilipoizaba 2-1 Cotonsport ya Cameroon, Juni 20, 2021.
Kikosi cha Simba SC kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam kesho Alhamis (Februari 09) alfajiri, kuelekea mjini Conakry-Guinea kupitia Adis Ababa-Ethiopia.