Boniface Gideon – Mara.
Mwekezaji wa kiwanda chakuchakata zao la Alizeti, Nyihita Wilfred amewaomba Wakulima wa zao hilo kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya Kiwanda katika Kijiji Nyanchabakenye kilichopo Wilaya ya Rorya Mkoani Mara.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Nyihita alisema mahitaji ya Kiwanda hicho kwa siku ni Tani 24 lakini kwasasa wanapata asilimia 5 ya mahitaji ya Kiwanda alichokijenga kwa ajili ya kuchakata zao hilo ambapo pia ameweza kutoa ajira kwa vijana hatua ambayo ni ya kujivunia kwa Wakazi wa Wilaya hiyo.
Amesema, “niliigeuza changamoto na kuwa fursa kwake hii ni kutokana na kukosekana kwa kiwanda cha zao la Alizeti ndani ya mkoa huo na hivyo kupata wazo la kuja na sasa namiliki kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula yatokanayo na zao hilo jina lake ni Nyihita Sunflower Cooking oil Production.”
“Wakulima walianza kujiuliza maswali mara baada ya kulima mazao tutauza wapi nikapata wazo kwa kutafuta wazo la soko na kujenga kiwanda baada ya kuanza ujenzi huo kiwanda hiki kilizinfuliwa rasmi 2021 na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa na ndio kikaanza kufanya kazi mpaka sasa,” alisema Nyihita.
Mariam Hamis, ni miongoni mwa wakulima na wanufaika wakubwa wa zao la Alizeti iambaye amesema wamekuwa wakijihusisha na uzalishaji wa zao hilo kwa muda mrefu, lakini hawakuwahi kupata mafanikio kutokana na kukosa soko, hivyo kwasasa wanashukuru uwepo wa kiwanda hicho.
“Uwepo wa kiwanda hiki ni furaha kwetu wakulima kwasababu tayari tumepata uhakika wa kutosha kuhusu changamoto ya muda mrefu, tulikuwa hatujui ni wapi tutauza mazao yetu baada ya kuvuna sasa wakulima wote tumehamasika na tunanufaika vya kutosha na uwepo wa kiwanda,” alisema Mariam.