Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Zambia Power Dynamos, Mwenya Chipepo amesema Simba SC imewapa somo la kutosha kabla ya kuanza mshike mshike wa Ligi Kuu ya nchini kwao na michuano ya Kimataifa.

Power Dynamos, ilicheza dhidi ya Simba SC juzi Jumapili (Agosti 06) katika Tamasha la Simba SC na kukubali kichapo cha 2-0.

Kabla ya safari ya kurejea kwao Zambia Kocha Chipepo alisema wamepata kipimo kizuri kucheza na Simba SC ambayo ina wachezaji wengi wazuri na wenye uzoefu mkubwa, na kuongeza kuwa wanarudi Zambia kurekebisha mapungufu waliyoyaona kwenye mchezo huo.

“Tumefurahishwa sana na mchezo wetu dhidi ya Simba SC, tunaamini tumejifunza mambo makubwa sana kutoka kwao, hii itatusaidia katika msimu mpya ambao tumejipanga kutetea ubingwa wetu nyumbani Zambia.”

“Sitilii maanani sana katika suala la kufungwa, binafsi ninatanguliza sana somo kubwa ambalo tumelipata kutoka kwa wenzetu Simba SC, ninaamini wachezaji wangu wameona namna ya kupambana katika ngazi ya Kimataifa.” Alisema Chipepo.

Mabao ya Simba SC kwenye mchezo huo yalifungwa na nyota wao wapya Willy Onana aliyefunga kipindi cha kwanza na lingine likifungwa na kiungo Fabrice Ngoma kipindi cha pili.

Robertinho: Mbona mambo bado
Fasheni ya mapengo inawalipa jamii ya Warangi