Mwenyekiti ambaye amemaliza muda wake wa kuiongoza Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Rais wa Namibia Dkt. Hage Geingob amezitaka nchi wanachama kuhakikisha vijana wanapewa kipaumbele katika nyanja mbalimbali kwa ajili ya kuleta maendeleo.
 
Amesema kuwa robo tatu ya wananchi wa jumuiya hiyo wana umri chini ya miaka 27 na hivyo kundi hilo la vijana likipewa nafasi kwenye zao kuna uwezekano mkubwa kwa nchi hizo kupiga hatua.
 
Ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kabla ya kukabidhi uenyekiti wa SADC kwa Rais wa Serikali ya Tanzania Dkt. John Magufuli.
 
Aidha, amesisitiza kuwa robo tatu ya wananchi wa jumuiya hiyo ni vijana, hivyo wakitumika vizuri itasaidia kuleta maendeleo.
 
“Ukweli ni kwamba lazima twende pamoja na vijana wetu, tushirikiane kwa kila hatua, naamini vijana wakitumika kikamilifu nchi zetu zitapiga hatua kubwa kimaendeleo, tunayo changamoto ya ajira kwenye nchi zetu ambapo vijana wamekuwa wakikimbilia nchi za Ulaya, umefika wakati wa kuwashirikisha vijana kutatua changamoto zetu,” amesema Geingob
 
Mwenyekiti huyo aliyemaliza muda wake ameeleza haja ya nchi hizo kuweka mikakati ya kuboresha miundombinu na huduma za jamii kwa ajili ya wananchi huku akihimiza uongezaji thamani kwa mazao yanayozalishwa kwa nchi wanachama.
 
Wakati huo huo amesema kuwa kuna kila sababu ya kuongeza jitihada za kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafanikiwa huku akitumia nafasi hiyo kueleza Serikali za jumuiya hiyo kuwa na sera ambazo zinakuza uchumi wa wananchi na kwamba sekta binafsi zipewe nafasi ya kushiriki kuleta maendeleo.
 
Akizungumza zaidi kuhusu jumuiya hiyo Dkt. Geingob amesema kwamba nchi za SADC zinatambua na kuthamini mchango wa Baba wa Taifa la Tanzania Hayati Julius Nyerere kwa namna ambavyo alijitoa kufanikisha nchi nyingi za Afrika zinakuwa huru.
Hata hivyo, amezishukuru nchi za jumuiya hiyo namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana na kusaidiana kukabiliana na majanga yanayotokea na hasa vimbunga na mafuriko.
 
Amezitaka nchi za SADC kuhamasisha wananchi kutunza mazingira kwa kutokata miti hovyo na kuwahamasisha kupanda miti kwa wingi kama njia mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Marais wastaafu watinga katika mkutano wa SADC
Tanzania yapongezwa kwa kukidhi vigezo vya uchumi vya SADC