Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania ‘SPUTANZA’ Mussa Kisoki ameingilia kati sakata la Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal salum ‘Fei Toto’ dhidi ya klabu ya Young Africans, ambalo bado linaunguruma mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’.
Fei Toto jana Jumatano (April 12) alifika katika Ofisi za TFF kwa ajili ya kusikiliza Shauri lake dhidi ya Young Africans, ambalo linashinikiza kuvunjwa kwa mkataba kati yake na Uongozi wa klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kisoki amesema haoni upenyo kwa Fei Toto kutimiza lengo lake la kuondoka Klabuni hapo kwa shinikizo la kuvunjwa kwa Mkataba wake kutoka TFF, zaidi ya kusaka namna sahihi ambayo itamsaidia kuwafanya viongozi wa Young Africans kukubali kumwachia.
“Watu wengi sana wamekuwa wakilichukulia suala la Feisal kiushabiki zaidi. Kuanzia Mashabiki mpaka wachambuzi wanafanya hivyo. Mtu pekee ambaye naona alimshauri vyema Feisal ni Aden Rage.”
“Fei Toto anapaswa kufuata kanuni za FIFA Ili kuvunja Mkataba kwa hiyo anapaswa kurejea Young Africans na kifungu namba 15 cha FIFA ambacho kinaelezea namna ya kuvunja Mkataba”
“Namna pekee iliyobakia Kwa Fei Toto ni kwenda CAS au kurudi kukaa na Young Africans na sio Shirikisho ambapo kamati imeshatoa maamuzi yake.”
“Namshauri tu huyu dada anayemsimamia Fei Toto (Jasmine Razack) aache kumpotezea muda tu Fei Toto kwa kuwa hakuna namna TFF watamsaidia Mteja wake kuvunja Mkataba.”
“TFF wangemsaidia Fei Toto kuvunja Mkataba kama tu Mchezaji asingetimiziwa yaliyopo kwenye Mkataba wake” amesema Mussa Kisoki Shauri la Fei Toto dhidi ya Young Africans limesogezwa mbele na kutarajiwa kusikilizwa tena Mei 04, 2023 saa nne asubuhi.